Angola yapongeza ushirikiano na China katika kupanua uchumi wa nchi hiyo
2022-08-31 08:48:42| CRI

Waziri wa Uchumi na Mipango wa Angola, Mario Augusto Joao amesema, nchi hiyo inatafuta kupanua uchumi wake, na inakaribisha uwekezaji zaidi na ushirikiano kutoka China kwa kuwa fursa hiyo itakuwa ni ya kunufaishana.

Katika mahojiano yake hivi karibuni na Shirika la Habari la China Xinhua, waziri huyo amesema anuai ya kiuchumi, hususan kutoka kwenye sekta ya mafuta na kuingia kwenye sekta zisizo za mafuta imekuwa ni moja ya malengo makuu ya nchi hiyo katika miaka mitano iliyopita.

Waziri Joao amesema kilimo cha kibiashara, maendeleo ya mtaji wa watu na kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini Angola ni misingi mitatu muhimu wakati nchi hiyo ikiendelea na lengo lake la kupanua uchumi katika miaka mitano ijayo.

Amesema Angola ina eneo kubwa la ardhi, na amewakaribisha wawekezaji kutoka China kulima bidhaa za China na kuziuza nchini China, na hii inatokana na China kuondoa ushuru kwa mazao ya kilimo kutoka Afrika, na pia kuruhusu bidhaa za Angola kuingia kwenye soko la China.

Pia amesema, serikali itaongeza uwezo wa mtaji wa nguvukazi kwa kuboresha sekta za elimu na afya, kwa kuwa nguvukazi ni moja ya hitaji muhimu la waajiri katika uchumi.

Waziri Joao amesema, jambo lingine muhimu ni mazingira ya kibiashara, na kuongeza kuwa, watahakikisha kila mtu anaweza kuanzisha na kuendesha biashara yake, kuwa na uwezo wa kupata fedha, na kuwa mmoja wa wachangiaji wakuu wa uchumi wa nchi hiyo.