Sudan yawasiliana na balozi wa Ethiopia kufuatia taarifa kuhusu kudunguliwa kwa ndege
2022-08-31 08:45:57| CRI

Sudan imewasilisha malalamiko yake kwa Balozi wa Ethiopia nchini humo Yibeltal Aemero Alemu, kupinga taarifa yake kuhusu Ethiopia kuangusha ndege inayoshukiwa kutoka kwenye anga ya Sudan.

Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Fadl Abdullah Fadl amepinga taarifa iliyotolewa na Balozi Alemu ikithibitisha kuwa jeshi la Ethiopia limetungua ndege iliyobeba silaha kwa ajili ya kundi la Harakati za Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) baada ya ndege hiyo kupita kwenye anga ya Sudan na kuingia kwenye anga ya Ethiopia bila kibali.

Amesema tuhuma hizo ni tofauti na utamaduni wa kidiplomasia katika mawasiliano na mamlaka rasmi zinazohusika, hususan kwa kuwa uongozi wa nchi hizo mbili unatafuta kumarisha zaidi uhusiano wa pande hizo mbili.

Wiki iliyopita, jeshi la anga la Ethiopia lilitangaza kutungua ndege iliyobeba silaha kwa ajili ya waasi wa kundi la TPLF ambayo iliingia kwenye anga ya Ethiopia kupitia Sudan.