Waziri Mkuu mpya wa Uingereza asema atatoa kipaumbele kwenye uchumi, nishati na huduma za afya
2022-09-07 08:53:08| CRI

Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Bibi Liz Truss amehutubia taifa kwa mara ya kwanza baada ya kuchukua nafasi hiyo na kusema atatoa kipaumbele kwenye uchumi, nishati na huduma za afya.

Bibi Truss anakuwa Waziri Mkuu wakati Uingereza inakabiliana na msukosuko mkubwa wa kupanda kwa gharama za maisha, kutokana na bei za chakula na nishati kuendelea kuongezeka, na kufanya mfumuko wa bei uendelee kupanda tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Takwimu zinaonesha kuwa mwezi Julai faharisi ya bei ya bidhaa (CPI) ilipanda kwa asilimia 10.1, ikiwa imepita kwa kiasi kikubwa lengo la asilimia 2 lililowekwa na Benki Kuu ya Uingereza.

Wakati wa kampeni Bibi Truss aliahidi kupunguza kodi, kulegeza usimamizi mkali wa serikali na kutoa kipaumbele kwenye ongezeko la uchumi, lakini wataalam wanatilia shaka kama hatua hizo zinaweza kuwa na ufanisi wa kutosha, kutokana na ugumu wa hali ya sasa.