Xi atoa pongezi kwa maadhimisho ya miaka 74 ya kuanzishwa kwa Korea Kaskazini
2022-09-09 14:57:10| CRI

Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Rais Xi Jinping wa China leo amemtumia salamu za pongezi Kim Jong Un, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Korea (WPK) na mwenyekiti wa Tume ya Masuala ya Korea Kaskazini katika maadhimisho ya miaka 74 ya kuanzishwa kwa nchi hiyo.

Xi alisema katika miaka 74 iliyopita, watu wa Korea Kaskazini wameungana kwa karibu na WPK na kusonga mbele, wakipata mafanikio muhimu katika kukuza ujenzi wa kiujamaa.

Pia alisema katika miaka ya karibuni, wakiongozwa na kanuni na sera zilizowekwa katika mkutano mkuu wa nane wa WPK, watu wa Korea Kaskazini wamepata maendeleo mapya mara kwa mara katika kuendeleza uchumi na kuboresha maisha ya watu, pamoja na kupigana vita kwa ushindi dhidi ya janga la COVID-19, ambapo China, kama ndugu mzuri, jirani mwema na rafiki wa dhati wa Korea Kaskazini, inafurahia sana.

Aliongeza kuwa inaaminika kuwa chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Kim na WPK, watu wa Korea Kaskazini hakika wataendeleza harakati za kiujamaa za nchi hiyo katika kutafuta maendeleo mapya na kuiinua nchi kwenye ngazi mpya.