Mfumuko wa bei wapungua kwa miezi mitatu mfululizo nchini Ethiopia
2022-09-13 09:02:09| CRI

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Idara Kuu ya Takwimu (CSA), kiwango cha mfumuko wa bei nchini Ethiopia kimepungua hadi asilimia 32.5 mwezi Agosti, na kuashiria kuwa kiwango hicho kimepungua kwa miezi mitatu mfululizo nchini humo.

CSA ilifichua kuwa kiwango cha mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula kimepungua hadi asilimia 33.2 mwezi Agosti, ikilinganishwa na asilimia 35.5 mwezi Julai. Hata hivyo takwimu mpya zaidi za CSA, zinaonesha kiwango cha mfumuko wa bei usio wa vyakula bado unaendelea kuongezeka, na kufikia asilimia 31.5 mwezi Agosti, ambalo ni ongezeko la asilimia 1.1 kutoka takwimu za Julai.

Hivi karibuni mfumuko wa bei kwa ujumla ulipungua kutokana na serikali za mitaa na serikali kuu kuendelea na juhudi za kudhibiti shinikizo la mfumuko wa bei. Athari za janga la COVID-19, migogoro katika maeneo mbalimbali ya Ethiopia, bei ya juu ya mafuta duniani, pamoja na hali ya ukame inayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, zimerejesha nyuma kwa kiasi kikubwa juhudi za serikali za kukomesha mfumuko wa bei nchini humo.