Sudan Kusini kutoa chanjo ya surua kwa zaidi ya watoto 37,000
2022-09-13 08:42:36| CRI

Wizara ya Afya ya Sudan Kusini ikisaidiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) imesema imeanza kampeni yake ya kutoa chanjo ya surua inayolenga watoto 37,390 wenye umri kati ya miezi sita na miaka 14.

Kwenye taarifa yao ya pamoja, vyombo hivyo viwili vimesema kuwa zoezi linaendelea katika kaunti ya Juba ambayo imekuwa na historia ya kujirejea kwa ugonjwa huo, ambapo mlipuko mmoja ulithibitishwa mwaka 2017 na wa hivi karibu ni ule wa mwaka 2019. Kampeni hiyo inalenga kufikia angalau asilimia 95 ya watoto ili kuzuia maambukizi yanayoendelea ya virusi vya surua kwenye kaunti hiyo.

Kaimu mwakilishi wa WHO nchini Sudan Kusini, Fabian Ndenzako amesema ugonjwa wa UVIKO-19 umevuruga mipango ya kutoa chanjo duniani, na kuongeza hatari ya milipuko mikali ya magonjwa.

Naye mkurugenzi mkuu wa Wizara ya Afya katika jimbo la Equatoria ya Kati Jamal Hassen, amesema wizara yake inatoa huduma za chanjo bure dhidi ya magonjwa yanayoweza kukingwa na chanjo ili kuzuia watoto wasipate surua.