Mjumbe wa China atoa wito wa kufanyiwa marekebisho vikwazo vya Sudan
2022-09-14 10:16:29| CRI

Naibu mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Dai Bing ametoa wito wa kurekebishwa na mwisho kuondolewa kabisa vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Sudan kuhusiana na eneo la Darfur.

Amesema vikwazo hivyo vimezuia sana uwezo wa serikali ya Sudan kudumisha utulivu na kuwalinda raia huko Darfur, na kwamba hatua za vikwazo zinapaswa kurekebishwa kwa kuzingatia hali inayoendelea hadi vitakapoondolewa. Ameliambia Baraza la Usalama kuwa China inasikitika kwamba Baraza hilo halikuweza kuweka vigezo vya kurekebisha vikwazo dhidi ya Sudan hadi ifikapo Agosti 31, kama linavyoeleza azimio la Baraza la Usalama, na inawataka wadau kutekeleza majukumu kwa dhati, kuanza tena mashauriano haraka iwezekanavyo, na kufanya juhudi kubwa ili kufikia makubaliano.

Ameongeza kuwa lazima isisitizwe kwamba vigezo vinapaswa kuwa wazi, vilivyofafanuliwa vizuri na vya kweli. Havipaswi kwenda zaidi ya suala la Darfur na hatua zilizopo za vikwazo, wala visitumike kama chombo cha kisiasa cha kuchelewesha kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Sudan.