Uganda yalaani vikwazo vya EU dhidi ya maendeleo ya mafuta na gesi
2022-09-16 08:33:58| CRI

Bunge la Uganda limelaani azimio la bunge la Umoja wa Ulaya (EU) la kusitisha maendeleo ya sekta ya mafuta nchini humo, likitaja ni kutokana na wasiwasi wa mazingira na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Bunge la EU limezishauri Uganda na Tanzania kutoendelea na ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki litakalosafirisha mafuta kutoka magharibi ya Uganda hadi bandari ya Tanga, nchini Tanzania. EU pia ilizionya nchi wanachama kutotoa msaada wowote wa kidiplomasia, kifedha au mwingine kwa miradi ya mafuta na gesi ya Uganda.

Naibu spika wa bunge la Uganda Bw. Thomas Tayebwa amesema hoja ya bunge la EU inalenga kurudisha nyuma maendeleo ya mafuta na gesi ya Uganda pamoja na ukuaji wa kiuchumi na kijamii na maendeleo ya nchi hiyo kwa ujumla.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema mapato yatakayopatikana kutokana na mafuta hayo yatakuwa muhimu katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi ya nchi na kikanda.