UM kutoa mafunzo kwa wanawake na vijana wajasiriamali wa Afrika Mashariki kuhusu fursa zinazotokana na AfCFTA
2022-09-21 08:40:27| CRI

Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) limesema kuwa linashirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa kutoa mafunzo kwa wanawake na vijana katika kanda ya Afrika Mashariki kuhusu fursa za kibiashara zinazotolewa na Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFCT).

Katika taarifa yake, Baraza hilo limeyataja mashirika ya Umoja wa Mataifa yatakayoshirikiana nalo kuwa ni Kituo cha Kimataifa cha Biashara, Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Maendeleo ya Wanawake.

Taarifa hiyo imesema, Baraza hilo na mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yalifanya warsha ya siku tatu mjini Kampala, Uganda, kuanzia jana, ambapo zaidi ya wawakilishi 70 kutoka jamii ya wafanyabiashara wa kanda hiyo watajifunza kuhusu Eneo la Biashara Huria la Afrika na kupata uelewa wa hadhi ya majadiliano na pia maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa makubaliano ya kibiashara.