Mlipuko wa virusi vya Ebola watokea katikati ya Uganda
2022-09-21 08:43:05| CRI

Wizara ya Afya nchini Uganda imesema, mlipuko wa virusi hatari vya Ebola umetokea katikati ya nchi hiyo.

Wizara hiyo imesema, mtu mmoja aliyelazwa katika hospitali ya mkoa wa Mubende alhamis iliyopita baada ya kuonyesha dalili za Ebola alifariki jumatatu wiki hii na kuongeza kuwa, vifo vingine sita vinachunguzwa baada ya jamii za eneo hilo kuripoti watu kufariki kutokana na ugonjwa wa ajabu.

Mwezi uliopita, Uganda iliimarisha ufuatiliaji kwenye mpaka wake wa magharibi baada ya Shirika la Afya Duniani kutangaza kutokea kwa kisa cha Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Wizara ya Afya ya Uganda imesema hatari ya kuenea kwa magonjwa iko juu katika wilaya 21 zinazopakana na eneo hilo.

Uganda imeshuhudia milipuko mitano ya Ebola katika miongo miwili iliyopita, hasa katika maeneo yake ya magharibi karibu na DRC.