Wataalamu wa China na Afrika watoa wito wa kutumia mfumo wa asili wa chakula
2022-09-22 08:56:39| CRI

Wataalamu wa China na Afrika wamesema, matumizi makubwa ya  mfumo wa asili wa chakula ni ufunguo wa kukabiliana na migogoro ya mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa anuwai ya baiolojia na uchafuzi wa hewa.

Wakizungumza katika mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao jana, wataalamu hao wamesema kuhama kutoka mifumo ya kilimo inayotegemea kemikali na kuingia kwenye  mfumo wa kilimo ulio rafiki wa mazingira kunaweza kuwa jawabu la uharibifu wa mazingira, uchafuzi mkubwa wa hewa na mashinikizo yanayotokana na hali ya hewa yanayozikabili jamii za kusini mwa dunia.

Mkuu wa Pendekezo la Asili la China katika Jukwaa la Uchumi la Dunia, Zhu Chunquan amesema, afya ya dunia itadumishwa mara mifumo ya uzalishaji wa chakula itakapoendana na kuboreshwa kwa ulinzi wa mifumo muhimu ya ikolojia ikiwemo misitu na vyanzo vya maji.

Mtafiti na Mtetezi katika Kituo cha Anuwai ya Baiolojia cha Afrika (ACB) Linzi Lewis amesema, thamani ya mnyororo wa kilimo kutoka uzalishaji, uhifadhi, usambazaji na matumizi inapaswa kuendana na  mazingira ya kijani, kupunguza hewa chafu zinazotolewa katika bustani za ndani zinazodhuru mazingira.