Zambia na China kuandaa jukwaa la biashara na uwekezaji
2022-09-22 08:55:47| CRI

Zambia na China zinaandaa Jukwaa la kwanza la biashara na uwekezaji linalolenga kufungua fursa za biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

Jukwaa la Biashara na Uwekezaji litafanyika mjini Lusaka, Zambia, kuanzia tarehe 28 hadi 29 mwezi Septemba, chini ya kaulimbiu ya “Uwekezaji kati ya China na Zambia katika zama mpya: Mazingira yote, Mbinu zote, na Urafiki Bora.”

Akizungumza jana mjini Lusaka, Kaimu Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zambia Elias Mubanga  alisema kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni ishara ya uhusiano imara uliopo kati ya nchi hizo mbili kwa miaka kadhaa, na jukwaa hilo  litatoa fursa na kutumika kama hatua kubwa ya kuendeleza uhusiano wa kiuchumi kati ya China na Zambia.

Naye Balozi wa China nchini Zambia, Du Xiaohui amesema, pande hizo mbili zitasaini makubaliano matatu ya awali kwa ajili ya ushirikiano mkubwa katika uwekezaji, uchumi wa kidijitali, na uwekezaji pamoja na mazingira mazuri ya ushirikiano wa kiuchumi.

Balozi Du amesema, biashara kati ya pande hizo mbili katika nusu ya kwanza ya mwaka huu imefikia dola za kimarekani bilioni 3.76, ikiwa ni ongezeko la asilimia 40 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.