Rais wa Kenya atoa amri ya kuunda kikosi kazi cha kukabiliana na madhara ya ukame
2022-09-26 08:54:12| CRI

Rais William Ruto wa Kenya amemwagiza naibu wake Bw. Rigath Gachagua kuunda kikosi kazi cha kukabiliana na madhara ya ukame nchini Kenya.

Rais Ruto ametoa agizo hilo jana kwenye Ikulu ya Kenya wakati akihutubia taifa kutoa shukrani kufuatia ushindi wake kwenye uchaguzi wa rais uliofanyika Agosti 9.

Kenya ni moja ya nchi za pembe ya Afrika zilizoathiriwa na ukame mkali unaowaathiri watu milioni 36. Umoja wa Mataifa umesema watu milioni 24.1 nchini Ethiopia, milioni 7.8 nchini Somalia na milioni 4.2 nchini Kenya wataathiriwa na ukame mkali katika mwezi Oktoba.

Ofisi ya uratibu wa maswala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema idadi hiyo imeongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa jumla ya waathirika milioni 19.4 ya mwezi julai.