AU yazindua vituo vya pamoja vya operesheni ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya kundi la al-Shabab nchini Somalia
2022-10-10 08:58:02| CRI

Tume ya Mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia imefungua vituo vya pamoja vya operesheni ili kuimarisha uratibu na mipango kwa kushirikiana na vikosi vya usalama vya Somalia wakati wa operesheni dhidi ya kundi la al-Shabab.

Kamanda wa Tume hiyo Diomede Ndegeya amesema, vituo hivyo vitawezesha vikosi husika kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha operesheni za ufanisi dhidi ya wapiganaji wa al-Shabab.

Amesema maofisa wa Tume hiyo, vikosi vya ulinzi vya Somalia, na wadau husika watafanya uratibu na kupanga operesheni katika vituo hivyo, na kuwataka makamanda wa sekta zote kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika maeneo yao ya operesheni kwenye mikoa husika.

Ameongeza kuwa, vituo hivyo vinaunga mkono utekelezaji wa maazimio kadhaa ya Umoja wa Mataifa yanayotaka vikosi vya usalama nchini Somalia kuchukua wajibu kamili hatua kwa hatua, kulinda usalama wa nchi hiyo.