Mawaziri wa Afrika waahidi kuanzisha mpango wa maendeleo ili kuimarisha usalama wa chakula
2022-10-12 08:25:54| CRI

Mawaziri wanane kutoka nchi za Pembe ya Afrika wameahidi kuendeleza mpango wa kina utakaosaidia kuongeza usalama wa chakula wakati ukame ukitishia baadhi ya nchi za kanda hiyo.

Taarifa iliyotolewa jana jijini Nairobi, Kenya, na Shirika la Maendeleo ya Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) imesema, uhaba wa mvua kwa misimu minne mfululizo katika miaka mitatu iliyopita umeziathiri zaidi jamii katika maeneo ya jangwa na nusu jangwa, ambazo ziko hatarini zaidi na kutokea tena kwa ukame.

Mawaziri hao na viongozi wa ujumbe kutoka nchi wanachama wa IGAD waliomaliza mkutano wao wa siku mbili mjini Nairobi, wamesema mpango huo utatoa kipaumbele katika kuongeza juhudi za kuzuia njaa, kuimarisha mifumo ya chakula, kuongeza unyumbufu na kuboresha biashara ya kuvuka mpaka ndani ya kanda hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika hilo, karibu watu milioni 50 katika Pembe ya Afrika wako hatarini kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula itakapofika mwisho wa mwaka huu.