Polisi nchini Kenya yaimarisha operesheni ya kuwasaka al-Shabaab baada ya uvamizi
2022-10-24 09:39:33| CRI

Polisi nchini Kenya imeimarisha operesheni za usalama katika mji wa Mandera uliopo mkoa wa Kaskazini Mashariki mwa Kenya, na kuwasaka wapiganaji wa al-Shabaab waliovamia misikiti miwili na baadaye kutoa hotuba mbele ya waumini waliomo ndani kabla ya kuondoka.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kaskazini Mashariki George Seda amesema wapiganaji hao walibeba bunduki aina ya AK47 na kwenda kwenye misikiti ya Elram A na B wakati wa sala ya alfajiri Jumamosi na kuwaambia waumini waliokuwepo misikitini kuwa wapo kwenye vita na watu wasio waislamu na kuwataka wajiunge na vita hivyo. Kwa mujibu wa Seda hakuna aliyejeruhiwa kwenye tukio hilo.

Habari nyingine zinasema, huko nchini Somalia limetokea shambulio la gari lililotegwa mabomu ambalo lililenga hoteli maarufu katika mji wa Kismayo uliopo kusini mwa nchi hiyo siku ya Jumapili. Naibu Mkuu wa polisi wa Jubaland Mohamed Nasi Guled amesema washambuliaji walivamia Hoteli ya Tawakal kwa gari lililosheni vilipuzi, na kurushiana risasi na vikosi vya usalama. Hata hivyo hakutoa idadi ya watu waliojeruhiwa au kufa. Kundi la kigaidi la Al-shabab limetangaza kuhusika na shambulio hilo.