Safaricom ya Kenya yashirikiana na Huawei kuzindua mtandao wa 5G
2022-10-28 09:49:52| CRI

Ofisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Safaricom Bw. Peter Ndegwa amesema kuwa kampuni hiyo imeshirikiana na kampuni ya teknolojia ya China Huawei kuzindua mtandao wa 5G wa kibiashara nchini humo.

Bw. Peter amesema kuwa sasa Kenya ina vituo 35 vya 5G vilivyosambazwa mjini Nairobi, Kisumu, Kisii, Kakamega na Mombasa, na inapanga kuongeza hadi vituo 200 nchini kote kufikia mwezi Machi, mwakani. Amesema wanaamini nguvu ya mageuzi ya mtandao wa internet itaendelea kutoa teknolojia ya hali ya juu zaidi ili kuwezesha wateja kufurahia maisha ya kidijitali.

Ofisa Mkuu Mtendaji wa Huawei Kenya Bw. Will Meng amesema kuwa watumiaji wa Kenya wanatazama zaidi televisheni za HD, kucheza michezo zaidi ya mtandaoni, kufanya kazi wakiwa nyumbani, na hivyo kutumia data zaidi na zaidi ya mtandao.

Bw. Meng ameeleza kuwa kwa zaidi ya miaka 20, Huawei imesaidia kujenga mitandao nchini kote Kenya. Ameongeza kuwa Huawei nchini Kenya pia itaongeza uwezo wake wa kimataifa katika 5G kusaidia Safaricom na Kenya kutumia vyema 5G ili kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii.