Wakimbizi takriban 90 waliokimbia mapigano DRC wafika Rwanda
2022-11-15 10:20:30| CRI

Meya wa wilaya ya Rubavu, magharibi mwa Rwanda Bw. Kambogo Ildephonse jana alisema wakimbizi takriban 90 waliokimbia mapigano huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamefika Rwanda.

Alisema Jumapili mchana waliwapokea raia 89 wa DRC kutoka familia 33, wakiwemo watoto zaidi ya 50. Watu hao waliripotiwa kukimbia mapambano kati ya jeshi la serikali na waasi wa M23. Wakimbizi hao watasitiriwa na familia za Rwanda kwa muda, lakini kuna mpango wa dharura wa kuwasaidia huku wakiendelea kufuatilia hali zao.

Habari zimesema wakimbizi hao waliingia Rwanda kupitia kituo cha mpakani cha Kabuhanga kilichoko kwenye eneo la Rubavu wakiripotiwa kukimbia mapambano yaliyotokea Jumapili huko Ruhunda na Buhumba, mashariki mwa DRC. Umoja wa Mataifa umesema mapambano mapya kati ya jeshi la DRC na waasi wa M23 yamesababisha hali mbaya ya kibinadamu yenye utatanishi.