Mkutano kati ya wakuu wa China na Marekani watajwa kufikia lengo lililotarajiwa
2022-11-15 15:28:17| CRI


 

Rais Xi Jinping wa China jana alasiri alikutana na mwenzake wa Marekani Joe Biden kisiwani Bali nchini Indonesia.

Baada ya mkutano wao kumalizika, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bw. Wang Yi alipokutana na wanahabari alisema, mkutano huo umefikia lengo lililotarajiwa la kuimarisha mawasiliano, kuweka bayana madhumuni na mstari mwekundu, kuepusha migogoro, kuonesha mwelekeo na kutafuta ushirikiano.

Bw. Wang Yi amesema, mkutano huo uliofanyika kutokana na pendekezo la Marekani, ni wa kwanza kati ya wakuu wa China na Marekani katika miaka mitatu iliyopita, ni wa kwanza tangu rais Biden aingie madarakani, na pia ni wa kwanza kati ya wakuu wa nchi hizo mbili baada ya kila upande kukamilisha ajenda yake muhimu ya ndani.

Bw. Wang Yi amebainisha kuwa, mkutano huo uliodumu kwa saa tatu, si kama tu una umuhimu mkubwa kwa hali ya sasa, bali pia utatoa athari ya kina kwa uhusiano wa nchi hizo mbili katika kipindi kijacho na hata mbele zaidi. Mkutano huo umetoa mwelekeo wa kuepusha uhusiano kati ya China na Marekani usiingie kwenye hali ya kutodhibitika na kutuliza uhusiano wa pande hizo. Katika hatua zijazo, pande hizo mbili zitadumisha mawasiliano, kudhibiti tofauti zao na kuhimiza ushirikiano, ili kuleta utulivu na kupunguza sintofahamu katika dunia ya leo.