Marais wa China na Mongolia wafanya mazungumzo
2022-11-29 08:53:09| CRI


 

Rais Xi Jinping wa China leo amefanya mazungumzo na mwenzake wa Mongolia Ukhnaagiin Khurelsuh ambaye yuko ziarani nchini China. Rais Xi amesema nchi hizo mbili ni majirani, na kudumisha uhusiano wa  ujirani mwema wa muda mrefu kunaendana na maslahi ya kimsingi ya nchi hizo na watu wao.

Rais Xi amesisitiza kuwa ushirikiano wa sekta mbalimbali kati ya nchi hizo mbili umeendelea kuimarika, na kuwa mfano wa kuigwa kwa uhusiano kati ya nchi. Ameongeza kuwa China inapenda kushirikiana na Mongolia kusukuma mbele maendeleo ya uhusiano wao wa wenzi wa kimkakati katika pande zote, ili kunufaisha watu wao.

Rais Khurelsuh amesema anapenda kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi yake na China, kujenga kwa pamoja “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, kupanua na kuimarisha ushirikiano katika sekta za uchumi na biashara, uwekezaji, nishati, madini, miundombinu, mabadiliko ya tabia nchi, maendeleo endelevu na udhibiti wa kuenea kwa majangwa, na kusukuma mbele ujenzi wa Eneo la kiuchumi la China-Mongolia-Russia.

Pande hizo mbili zimetoa taarifa ya pamoja zikikubaliana kushirikiana katika ujenzi wa mambo ya kisasa, na kujitahidi kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja ya kuishi pamoja kwa amani, kusaidiana na kushirikiana ili kupata mafanikio ya pamoja.