Maambukuzi ya Ebola nchini Uganda yapungua kutokana na hatua kali za udhibiti
2022-11-29 08:52:24| CRI

Hatua kali za udhibiti wa Ebola, ikiwa ni pamoja na kufungwa haraka kwa eneo la mlipuko wa ugonjwa huo, zimekuwa na matokeo chanya na kufanya  maambukizi ya ugonjwa huo nchini Uganda kupungua.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema kwenye taarifa yake  iliyosomwa na Makamu wake Jessica Alupo, kuwa zuio la muda wa siku 42 lililowekwa katika wilaya za Mubende na Kassanda, ambazo ni kiini cha mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda, zimepunguza ueneaji wa ugonjwa huo katika maeneo mengine ya Uganda hasa katika maeneo yenye watu wengi.

Rais Museveni amesema wizara ya afya ya Uganda ilikuwa na mwitikio wa haraka katika wilaya ambazo maambukizi yaliripotiwa, akitoa mfano wa mji wa Jinja, ambapo watu 300 ambao waliowasiliana na mgonjwa wa Ebola waliwekwa karantini.

Hadi kufikia Novemba 26, watu 141 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya Ebola, 79 wamepona na 55 wamekufa.