Mkutano wa kumwomboleza hayati Jiang Zemin kufanyika tarehe 6
2022-12-01 20:30:53| cri

Kamati ya Mazishi ya aliyekuwa rais wa China hayati Jiang Zemin imetoa tangazo leo tarehe 1 Desemba kuwa, kutokana na mchango mkubwa aliyetoa hayati Jiang katika maendeleo ya kihistoria ya chama na nchi, pamoja na matarajio ya pamoja ya chama, jeshi na watu wa makabila mbalimbali nchini China, kamati hiyo imeweka uamuzi ufuatao:

Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, Kamati ya Kudumu ya Bunge la Umma la China, Baraza la Serikali, Baraza la Mashauriano ya Kisiasa, na Kamati Kuu ya Kijeshi zitaandaa mkutano wa kumwomboleza hayati Jiang katika Jumba la Mikutano ya Umma la China saa nne asubuhi ya tarehe 6 Desemba.

Siku ambayo mkutano huo utakapofanyika, bendera kote nchini, pamoja na balozi na mashirika mengine ya China katika nchi za nje zitapeperushwa nusu mlingoti, na shughuli za burudani za umma zitasitishwa kwa siku moja.

Wakati mkutano wa maombolezo utakapofanyika, watu kote nchini watakaa kimya kwa dakika tatu, honi za magari, meli na treni zitapigwa kwa dakika tatu, na kengele za ulinzi wa umma zitalia kwa dakika tatu.