Kampuni za China zafanya maonyesho ya ajira kwa wanafunzi nchini Kenya
2022-12-14 10:09:33| CRI

Kampuni za China nchini Kenya zimefanya maonyesho ya siku mbili ya ajira katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, na kutoa nafasi za ajira kwa wanafunzi kutoka Kenya.

Maonyesho hayo yameandaliwa na Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Nairobi na kushirikisha kampuni 21 za China zinazofanya shughuli zao nchini Kenya.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho katika masuala ya Elimu Julius Ogeng’o amesema, maonyesho hayo yametoa fursa kwa wanafunzi kuwasiliana na waajiri watarajiwa, na hivyo kuongeza uwezekano wa kupata ajira. Ameongeza kuwa, kampuni za China zimejitokeza kuwa waajiri wazuri kwa kuwa wana utamaduni wa kuajiri wazawa katika kampuni zao.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Nairobi Wang Shangxue amesema, zoezi hilo la ajira linaziwezesha kampuni za China kuchagua wanafunzi bora wa Kenya kufanya kazi katika kampuni hizo.