Rais wa Zimbabwe asema uwekezaji zaidi unakaribishwa katika sekta ya madini
2022-12-16 09:10:06| CRI

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amesema nchi hiyo inakaribisha wawekezaji zaidi kuchukua fursa katika utafiti na uchimbaji, na faida za maliasili ili kuongeza thamani ya utajiri wake mkubwa wa madini.

Rais Mnangagwa amesema hayo wakati wa hafla rasmi ya uwekaji wa jiwe la msingi katika mgodi wa Sabi Star Lithium Wilayani Buhera, Mkoa wa Manicaland.

Kampuni ya Chengxin Lithium Group, yenye makao yake makuu nchini China, mwaka jana ilipata asilimia 51 ya hisa katika mgodi huo ulioko mashariki ya Zimbabwe.

Rais Mnangagwa amesema, uwekezaji huo utasaidia sana katika azma ya nchi hiyo kuanzisha viwanda vya madini ya lithiamu na mnyororo wa thamani.