Rasimu ya makubaliano ya UM yataka misaada zaidi kwa nchi zinazoendelea katika uhifadhi wa bioanuwai
2022-12-19 09:23:07| CRI

Rasimu ya makubaliano ya Umoja wa Mataifa juu ya uhifadhi wa bioanuwai inataka nchi zilizoendelea kuongeza misaada ya kifedha kwa nchi zinazoendelea hadi kiasi kisichopungua dola za kimarekani bilioni 20 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025 na kuongeza fedha hizo hadi zifikie dola bilioni 30 kwa mwaka ifikapo mwaka 2030. Misaada hiyo italenga hasa kwa nchi zilizo nyuma kimaendeleo na nchi zinazoendelea za visiwa vidogo, pamoja na nchi zenye uchumi wa mpito.

Rasimu hiyo iliyotolewa na China ambayo ni mwenyekiti wa mkutano wa COP15 wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Bioanuwai, inajumuisha malengo 23 yatakayotekelezwa kwa dharura katika muongo huu hadi mwaka 2030.

Mkutano wa COP15 umepangwa kuhitimishwa Jumatatu wiki hii kwa kupitishwa kwa mfumo wa kimataifa wa anuwai ya viumbe hai baada ya 2020. Rasimu hiyo imejadiliwa katika siku mbili zilizopita.