Kundi la M23 lajiondoa kwenye maeneo muhimu linayoyakalia Kaskazini Mashariki mwa DRC
2022-12-26 08:54:57| CRI


 

Kikosi cha kikanda cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Ijumaa kiliudhibiti rasmi mji wa Kibumba, ulioko umbali wa kilomita 20 kutoka Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambao hapo awali ulitekwa na waasi wa M23.

Kujiondoa kwa kundi la M23 huko Kibumba kulikuja baada ya mkutano wa pamoja uliofanyika Kibumba kati ya M23, maofisa wa jeshi la kikanda la EAC wakiongozwa na Jenerali wa Kenya Jeff Nyagah na baadhi ya wajumbe wa Mfumo wa Pamoja wa Kuthibitisha Kanda ya Maziwa Makuu.

Kwa niaba ya mamlaka ya kanda hiyo, Jenerali Nyagah aliwapongeza M23 kwa kujiondoa kwa amani, akilitaka kundi hilo kufanya vivyo hivyo katika maeneo mengine ambayo bado linayashikilia katika eneo hili la nchi ili kuharakisha mchakato wa amani. Aidha amewataka wakazi wa Kibumba kurejea majumbani mwao, na kuthibitisha azma ya jeshi la kikanda kutimiza wajibu wake kwa heshima ya uhuru na katiba ya DRC.