UM wasema watu 30,000 wamekimbia makazi yao Sudan Kusini kutokana na mapigano
2022-12-30 09:12:22| CRI


 

Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema takriban watu 30,000 wamekimbia makazi yao kufuatia mapigano katika eneo la Utawala la Greater Pibor.

Katika taarifa yake aliyoitoa huko Juba, Sudan Kusini, Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu nchini Sudan Kusini, Sara Beysolow Nyanti amesema shambulizi lililofanywa Disemba 24 na vijana wenye silaha kutoka Jimbo la Jonglei dhidi ya jamii za eneo la Utawala la Greater Pibor lilisababisha uvamizi wa mifugo, uharibifu wa mali na watu 5,000 kuhama makazi yao, wakiwemo wanawake na watoto waliokimbilia mji wa Pibor kutoka maeneo yenye migogoro ya Gumuruk na Lekuangole.

Nyanti ameeleza kuwa washirika wa kibinadamu wanatoa msaada unaohitajika kwa wale walioathiriwa na vurugu, na kuongeza kuwa mapigano ya hivi karibuni yamesababisha uhamaji mwingine mkubwa wa raia, uliochochewa na mapigano yaliyotokea katikati ya Novemba mwaka 2022 katika Kaunti ya Fashoda, Jimbo la Upper Nile.