Watu 14 wafariki katika ajali ya barabarani iliyotokea mkoani Mtwara, Tanzania
2022-01-04 08:44:50| CRI

Watu 14 wamekufa na wengine 22 wamejeruhiwa katika ajali ya lori kuparamia watu iliyotokea katika wilaya ya Newala mkoani Mtwara, Kusini mwa Tanzania.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara Bw Marc Njera, amesema ajali hiyo ilitokea Jumapili baada ya lori kuwaparamia watu waliokuwa wakishiriki kwenye sherehe ya jadi katika kijiji cha Lindumbe. Amesema baada ya ajali hiyo, dereva wa lori alikwenda kuegesha lori hilo kwenye kituo cha mafuta na kutoweka. Polisi wanamsaka dereva huyo.

Ofisa wa afya wa wilaya ya Newala Bw. Mohamed Halifa amesema watu nane kati ya waliojeruhiwa wako mahututi.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa salama za rambirambi kwa mkuu wa mkoa wa Mtwara Bw. Margo Gaguti, na kusema amesikitishwa na vifo vya watu hao wasio na hatia, na kuwatakia majeruhi wapone haraka.