Idadi ya kesi za COVID-19 barani Afrika yazidi milioni 10
2022-01-10 08:34:52| CRI

Idadi ya kesi za COVID-19 barani Afrika yazidi milioni 10_fororder_6

Idadi ya kesi zilizothibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona barani Afrika imepita milioni 10, huku virusi vya Omicron vikienea kwa kasi na kugundulika katika nchi 33 za bara hilo.

Takwimu zilizotolewa jana jumapili na Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa CDC) zimeonyesha kuwa, mpaka kufikia jumamosi jioni, idadi ya kesi zilizothibitishwa kuwa na virusi vya Corona barani humo ilifikia 10, 028,508, huku idadi ya vifo ikiwa ni 231, 157.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Madaktari la Afrika Kusini Dr. Angelique Coetzee amesema, ongezeko la kasi la maambukizi huenda limetokana na virusi vilivyobadilika vya Omicron.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika, Dr Matshidiso Moeti amesema, huu ni wakati muhimu wa kupambana na janga la COVID-19, na uzembe wowote ni adui mkubwa. Ameongeza kuwa, kutokana na kuanza kuongezeka kwa upatikanaji wa vifaa, ni lazima kuongeza ufuatiliaji katika vikwazo vingine vya upatikanaji wa chanjo.