Msomi wa China: Kushikilia maendeleo ya kijani ni dhana muhimu ya ushirikiano kati ya China na Afrika
2022-01-10 08:48:09| CRI

Msomi wa China: Kushikilia maendeleo ya kijani ni dhana muhimu ya ushirikiano kati ya China na Afrika_fororder_王珩-浙师大非洲研究院党总支书记

Naibu mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Afrika ya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang Profesa Wang Heng amesema, China na Afrika zote zinakabiliwa na changamoto kubwa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, kwa hivyo kushikilia maendeleo ya kijani imekuwa dhana muhimu ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Akiongea kwenye kongamano moja lililofanyika hivi karibuni kuhusu matokeo ya mkutano wa nane wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC, Profesa Wang Heng amesema, Azimio la Ushirikiano wa China na Afrika Katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi lililotolewa kwenye mkutano wa Dakar wa FOCAC na Mpango wa Utekelezaji wa Dakar 2022-2024 vimesisitiza kuwa China na Afrika zimeamua kuanzisha uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika zama mpya, na pia vimeweka bayana kuwa China itatekeleza miradi kumi ya maendeleo ya kijani, uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya Afrika, na pia itaendelea kuongeza nguvu katika kuzijengea nchi za Afrika uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kujitahidi kujenga na kukamilisha kwa pamoja mifumo ya uchumi wa kijani, ili kukabiliana kwa pamoja na mabadiliko ya tabianchi.

Profesa Wang Heng amebainisha kuwa kuhimiza maendeleo ya kijani si kama tu ni moja ya mapendekezo manne yaliyotolewa kwenye mkutano wa Dakar, bali pia ni moja ya miradi tisa ya ushirikiano katika mpango wa kwanza wa miaka mitatu wa Ajenda ya Ushirikiano wa China na Afrika ya mwaka 2035. Kabla ya hapo, maendeleo ya kijani pia yalikuwa maudhui muhimu kwenye Mipango Kumi ya Ushirikiano iliyotolewa kwenye mkutano wa kilele wa FOCAC uliofanyika mwaka 2015 huko Johannesburg, na Hatua Nane zilizotangazwa kwenye mkutano wa FOCAC wa Beijing uliofanyika mwaka 2018. Hali hii imedhihirisha hadhi muhimu na uzito wa kimkakati wa maendeleo ya kijani kwenye ushirikiano kati ya China na Afrika. Ameongeza kuwa, hadi kufikia mwezi Septemba mwaka 2021, nchi saba za Afrika zikiwemo Angola na Kenya zimejiunga na Muungano wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kijani ya “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, na kutoa mchango chanya katika ujenzi wa njia ya hariri ya kijani. Aidha, China pia imejitahidi kuendeleza ushirikiano wa Kusini-Kusini kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambapo mpaka sasa imesaini nyaraka 15 za ushirikiano na nchi 14 za Afrika, na kuiunga mkono Afrika kutatua changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, kupitia kutekeleza miradi ya kupunguza kasi na kuhimili mabadiliko ya tabianchi, kujenga kwa pamoja maeneo ya mfano ya uchumi wa kijani na kutoa mafunzo ya kujenga uwezo na kadhalika.

Profesa Wang Heng anaona, ushirikiano wa Kusini-Kusini kwenye masuala ya tabianchi ukiwa ni sehemu muhimu ya misaada ya China kwa nje, ni nyanja ya kipaumbele kwenye diplomasia ya tabianchi, mazungumzo ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na vilevile kwenye ujenzi wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”. Amesema China na nchi za Afrika zinapaswa kubeba wajibu wao kulingana na viwango vyao vya maendeleo na hali halisi ya nchi, kufanya mjadala wa sera, mabadililishano ya watu na utafiti wa pamoja, ili kusukuma mbele mchakato wa kuboresha usimamizi wa mazingira na kuhimiza maendeleo endelevu katika China na Afrika.