Msomi wa Tanzania: Njia ya China yatoa chaguo jipya lililo tofauti na “Mwafaka wa Washington”
2022-01-12 13:56:17| CRI

Msomi wa Tanzania: Njia ya China yatoa chaguo jipya lililo tofauti na “Mwafaka wa Washington”_fororder_UNIT74_Prof Moshi

Mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa China katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Humphrey Moshi amesema, maendeleo ya kasi na shirikishi yaliyopatikana China katika muongo uliopita hayajawahi kushuhudiwa kote duniani, ambayo yamedhihirisha wazi kuwa, njia ya China imekuwa mbinu mpya ya maendeleo iliyo tofauti na “Mwafaka wa Washington (Washington Consensus)”, na kutoa chaguo jipya kwa nchi zinazoendelea.

Akihojiwa hivi karibuni na Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG, profesa Moshi amesema, China ni mwenza wa nchi za Afrika kwenye nyanja mbalimbali, mafanikio iliyoyapata China katika miaka 10 iliyopita yanatia moyo, na njia yake ya maendeleo imethibitisha kuwa, maendeleo ya uchumi na jamii yanaweza kutimizwa ndani ya kizazi kimoja, endapo uongozi sahihi wenye maono ya muda mrefu, unaozingatia maendeleo na kutoa kipaumbele kwa maslahi ya watu utakuwa katika nafasi yake. Uzoefu huo wa China unastahili kuigwa na nchi zote zinazoendelea, zikiwemo nchi za Afrika.

Alipozungumzia uhusiano kati ya Tanzania na China, profesa Moshi amesema, katika zaidi ya miaka 50 iliyopita, ushirikiano kati ya Tanzania na China umeendelea kuimarika, na kutoa athari chanya kwa maendeleo ya uchumi na jamii nchini Tanzania, ambapo kiwango cha miundombinu kimeinuka, maisha ya watu yameendelea kuboreka, huku juhudi za kupunguza umaskini zikiendelea kusonga mbele. Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025 vinalingana kwa kiwango kikubwa. Amebainisha kuwa, juhudi za kusukuma mbele maendeleo ya viwanda, ikiwa ni nyenzo muhimu ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za uchumi na jamii, zikiwemo kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira kwa vijana, mfumo dhaifu wa afya ya umma na kiwango cha chini cha ukuaji wa uchumi, zimepata maendeleo kiasi, lakini bado zinahitaji kutiliwa mkazo zaidi katika siku zijazo. Aidha, profesa Moshi anaona, ushirikiano wa pande hizo mbili unapaswa kutilia maanani zaidi maendeleo ya vijijini na kuongeza tija katika sekta ya kilimo, ili kuchangia zaidi kwenye juhudi za kupunguza umaskini, na kupanua ushirikiano kati ya sekta za kilimo na viwanda.

Profesa Moshi ameeleza kuwa, Baraza la Ushirikiano kati ya China FOCAC limepata mafanikio makubwa katika kuhimiza maendeleo ya uchumi na jamii tangu lilipoanzishwa. Mipango mipya iliyotolewa kwenye Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa FOCAC uliofanyika mwishoni mwa mwaka 2021 nchini Senegal, imeonesha uwezo na dhamira yake ya kuendana na mahitaji ya maendeleo ya Afrika, ambayo inahusisha nyanja mpya za ushirikiano, zikiwa ni pamoja na afya ya umma, teknolojia ya dijitali na mabadiliko ya tabianchi. Anaona kuwa, nyanja hizo mpya si kama tu zitaimarisha ushirikiano kati ya Afrika na China, bali pia zitaharakisha maendeleo ya uchumi na jamii barani Afrika.