Shirika la misaada la China latoa vifaa vya elimu katika jimbo lililoathiriwa na mafuriko nchini Sudan Kusini
2022-01-20 09:59:01| CRI

Wanafunzi ambao masomo yao yamekatizwa kutokana na mafuriko makubwa yaliyotokea katika Jimbo la Jonglei nchini Sudan Kusini wamepokea misaada ya vifaa mbalimbali vya elimu kutoka Mfuko wa China wa Kupunguza Umaskini CFPA ili kuendelea na masomo yao shuleni.

Balozi wa China nchini Sudan Kusini Hua Ning amekabidhi vifurushi zaidi ya 1,800 vilivyotolewa chini ya Mradi wa Panda Pack kwa maofisa wa Jimbo la Jonglei.

Amesema tangu uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili uanzishwe miaka 11 iliyopita, China siku zote inazingatia maendeleo ya elimu nchini Sudan Kusini. Pia ameeleza kuwa mfuko huo umekubali kupanua mradi wake nchini Sudan Kusini kwa mujibu wa mahitaji ya watoto.

Katibu mkuu wa serikali ya Jimbo la Jonglei Gatwech Koak Nyuon amewapongeza watu wa China kwa kuisaidia nchi hiyo, na kuongeza kuwa hatua hii imeonesha uhusiano mzuri kati ya nchi hizi mbili na kati ya wananchi wa nchi hizi mbili.