Mratibu mkazi wa UM: Ushirikiano wa China na Afrika una nguvu kubwa ya kushabihiana
2022-01-21 10:59:16| CRI

Mratibu mkazi wa UM: Ushirikiano wa China na Afrika una nguvu kubwa ya kushabihiana_fororder_联合国驻华协调员常启德在研讨会上致辞.JPG

Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini China Bw. Siddharth Chatterjee hivi karibuni amesema, China imetumia miaka 42 kujiendeleza kutoka nchi yenye pato la mtu mmoja (GDP per capita) sawa na dola za kimarekani chini ya 200 hadi kufikia kuwa uchumi mkubwa wa pili duniani, anaamini kuwa Afrika pia inaweza kupata mafanikio kama hayo ya China, kwa kuwa ushirikiano kati ya China na Afrika una nguvu kubwa ya kushabihiana.

Akihutubia Kongamano kuhusu kazi zijazo za Mkutano wa nane wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC lililofanyika tarehe 18 mjini Beijing, Bw. Chatterjee amesema ifikapo mwaka 2050, idadi ya watu barani Afrika inakadiriwa kufikia bilioni 2.5, milioni 890 kati yao wakiwa ni vijana, hali ambayo inaweza kuifanya Afrika kuwa soko kubwa zaidi la wazalishaji na wateja duniani. Ifikapo mwaka 2030, sekta ya afya na matibabu ya Afrika inakadiriwa kuongezeka hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 400, biashara ya sekta ya kilimo inaweza kufikia dola trilioni moja, huku uchumi wa buluu barani Afrika ukitarajiwa kufikia dola trilioni saba.

Ushirikiano wa China haukosekani kuiwezesha Afrika kutimiza malengo yake ya maendeleo. Bw. Chatterjee amesema, kuzinduliwa kwa ujenzi wa Eneo la Biashara Huria la Afrika ni fursa muhimu kwa maendeleo ya Afrika, na hivi sasa muunganiko wa miundobinu ya Afrika umeharakishwa kutokana na ushirikiano wa China. Akitolea mfano wa barabara ya kuunganisha mji mkuu wa Kenya Nairobi na mji wa mpakani kati ya Kenya na Ethiopia Moyale iliyojengwa na kampuni ya China, ameitaja kuwa barabara hiyo imeboresha kwa kiasi kikubwa maisha ya watu wa huko.

Akizungumzia maendeleo ya Afrika katika siku zijazo, Bw. Chatterjee  anaona, uwekezaji kwenye raslimali watu utakuwa ni moja ya nyenzo muhimu ya kuhimiza maendeleo barani Afrika na kutimiza Ajenda ya mwaka 2063 ya Umoja wa Afrika. Amesema, hivi sasa asilimia 70 ya watu wa Afrika ni vijana, kama watawezeshwa vya kutosha kwenye mambo ya elimu, ufundi stadi na ajira, anaamini kuwa Afrika pia inaweza kupata maendeleo makubwa kama iliyoyapata China katika miongo minne iliyopita.

Bw. Chatterjee amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unapenda kushirikiana na Umoja wa Afrika, nchi za Afrika na China katika kusukuma mbele uhusiano wa wenzi kati ya China na Afrika, na kutoa kichocheo kwenye majukwaa mbalimbali ya ushirikiano, ili kutoa msukumo endelevu kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa bara la Afrika.