Kenya yawapa uraia watu 14,000 waliochukuliwa kama wakimbizi
2022-01-21 10:23:55| CRI

Kenya jana Alhamisi iliondoa majina ya watu 14,000 ambao waliingizwa kwenye kanzi data ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) na kuwapa uraia.

Katibu Tawala wa Wizara ya Mambo ya Ndani Hessein Dhado, ameelezea mchakato wa kuondoa majina hayo kama hatua kubwa ya kuwalinda raia waliokuwa kwenye hatari ya kutokuwa na taifa. Dhado aliyekuwa akiongea katika mji wa Garissa kaskazini mashariki mwa Kenya, amesema kukabidhi uraia kwa raia wenyeji wanaochukuliwa kama wakimbizi ni kipaumbele cha kwanza.

Amefafanua kuwa watu wote walioondolewa hadhi ya ukimbizi watapatiwa haki za msingi kama vile elimu, afya, nyumba na kupata mtaji kutoka taasisi za mikopo ili kuwawezesha kufanya biashara. Kenya ilianza utaratibu wa kuondoa majina ya watu wanaochukuliwa kama wakimbizi tangu mwaka 2019 ili kuwawezesha kupata kadi ya utambulisho wa taifa na kushiriki katika shughuli za kiuchumi zenye tija.