Malori manane ya ujenzi pamoja na vifaa vya ujenzi vimechomwa moto na watu wanaotuhumiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab katika mji wa Hindi ulioko katika kaunti ya Lamu.
Kamishna wa kaunti ya Lamu Bw. Irungu Macharia, amesema malori hayo ni sehemu ya magari ya kampuni ya ujenzi ya China yanayotumika kwenye ujenzi wa barabara ya mradi wa LAPSSET. Bw. Macharia amesema hakuna majeruhi kwenye tukio hilo.
Amesema eneo hilo lina changamoto za mawasiliano ya simu, hali iliyofanya kuwa na ugumu wa kuwasiliana na polisi, lakini kwa sasa vikosi vya eneo hilo vinawasaka wahusika.
Taarifa za kiusalama zinasema watu waliokuwa wamesheheni silaha nzito walivamia eneo la maegesho saa kumi alfajiri na kupambana na askari wa jeshi la Kenya, lakini walifanikiwa kurusha mabomu ya petroli na kuchoma vifaa hivyo.