Ushirikiano kati ya China na Afrika kusukuma mbele maendeleo ya kijani barani Afrika
2022-01-25 15:12:17| CRI

Ushirikiano kati ya China na Afrika kusukuma mbele maendeleo ya kijani barani Afrika_fororder_WEI07039_w8718.JPG

Naibu mkurugenzi wa idara ya kimataifa katika Kamati ya taifa ya maendeleo na mageuzi ya China Bw. Gao Jian, amesema, Ruwaza ya mwaka 2035 iliyotolewa kwenye mkutano wa nane wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwaka jana, inaungana kwa karibu na Ajenda ya Mwaka 2063 ya Umoja wa Afrika, na itaiunga mkono Afrika kutimiza maendeleo shirikishi na ya kijani.

Akihutubia kongamano maalumu kuhusu kazi zijazo za Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa FOCAC lililofanyika hivi karibuni mjini Beijing, Bw. Gao Jian amesema, Ruwaza ya Mwaka 2035 ikiwa ni moja ya matunda makuu ya mkutano huo, ni mpango wa kwanza wa ushirikiano wa kipindi kirefu uliotungwa kwa pamoja na China na Afrika. Ruwaza hiyo inayoungana vizuri na Ajenda ya 2063 ya Afrika kwenye muundo wa sera, itaisukuma mbele Afrika kutimiza maendeleo shirikishi, endelevu na ya kijani.

Bw. Gao Jian amesema, katika usanifu wa ngazi ya juu, China imetoa dhana mpya ya maendeleo inayozingatia “uvumbuzi, uratibu, ukuaji wa kijani, uwazi na hali ya kunufaishana”, ambayo inalenga kufikia malengo ya maendeleo ya uchumi na jamii sambamba na kutimiza maendeleo ya kijani, na vilevile kuhakikisha usalama na upatikanaji wa nishati. China inapenda kutoa dhana hiyo kwa nchi za Afrika.

Bw. Gao Jian anaona, malengo ya kufikia kilele kwenye utoaji wa hewa ya ukaa na kutimiza uwiano kati ya utoaji na ufyonzaji wa hewa ya ukaa (carbon neutrality) yanahitaji matumizi ya nishati katika hatua za mwisho yawe ya kutumia umeme unaozalishwa kwa nishati endelevu. China na Afrika zina mustakbali mkubwa wa ushirikiano kwenye nyanja hiyo. Amesema, serikali ya China iliweka mipango kumi ya utekelezaji ya kufikia kilele kwenye utoaji wa hewa ya ukaa kabla ya mwaka 2030, ambayo inahusisha sekta za viwanda, mawasiliano, ujenzi, nishati na nyinginezo. Amesema, China inapenda kutoa uzoefu wake na usanifu wake wa sera kwa nchi za Afrika.

Bw. Gao Jian amesema, kutimiza maendeleo ya kijani kunahitaji pia ushirikiano wa karibu kati ya Sekta Binafsi na ya Umma. China na Umoja wa Afrika wameanzisha Utaratibu wa uratibu kuhusu ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, China inapenda kuhamasisha kampuni nyingi zaidi za China zenye teknolojia, uzoefu na mitaji kuwekeza zaidi katika nchi za Afrika chini ya utaratibu huo, ili kuisaidia Afrika kuongeza ajira, kuhimiza ukuaji wa uchumi, na kusukuma mbele maendeleo ya kijani barani humo.