Benki ya Dunia yatoa dola milioni 100 kwa waathirika wa mafuriko Sudan Kusini
2022-01-27 09:37:14| CRI

Benki ya Dunia imetangaza kutoa dola milioni 100 za kimarekani kwa waathirika wa mafuriko nchini Sudan Kusini.

Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayeshughulikia mambo ya Eritrea, Ethiopia, Sudan Kusini, Sudan, kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Bw. Ousmane Dione, amesema fedha hizo zitatolewa kwa serikali ya nchi hiyo katikati ya mwaka huu.

Bw. Dione amesema anaamini kuwa tatizo la mafuriko nchini Sudan Kusini litashughulikiwa kwa makini.

Tangu mwezi wa Mei mwaka jana, mafuriko mabaya yameathiri watu zaidi ya laki 8.4 katika majimbo saba nchini Sudan Kusini. Kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, mafuriko yanazidisha hali mbaya ya kibinadamu inayowakabili watu milioni 7.2, wakiwemo mamilioni ya watoto wanaokabiliwa na baa la njaa.