Kenya yatoa dozi milioni 12 za chanjo ya COVID-19 huku maambukizi yakipungua
2022-01-31 17:26:36| cri

Kenya imetoa zaidi ya dozi milioni 12 za chanjo ya COVID-19, ambapo asilimia 20 ya watu nchini humo imepata chanjo kamili.

Kwenye taarifa yake aliyoitoa jana Jumapili, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema kwamba serikali inalenga kuchanja asilimia 70 ya watu hadi kufikia mwezi Juni, ingawa maambukizi mapya na vifo vimepungua sana. Tangu Ijumaa, wizara ya afya ya Kenya imeanzisha kampeni ya wiki mbili ya kuchanja watu katika kaunti zote 47 nchini humo. Kwa mujibu wa waziri Kagwe wamesambaza timu takriban 3,000 za kutoa chanjo, pamoja na vituo 3,000 ambavyo sasa vinaendelea na zoezi la kutoa chanjo.

Kwa mujibu wa wizara ya afya, Kenya imeripoti wagonjwa wa COVID-19, 321,335 na vifo 5,580 hadi kufikia Jumapili, huku kiwango cha wagonjwa kikishuka hadi asilimia 2.6 kutoka cha juu zaidi ya asilimia 20 mwishoni mwa Disemba wakati maambukizi yalipovunja rikodi ya nyuma, yaliyochochewa na virusi vya Omicron.