Mkutano wa baraza tendaji la Umoja wa Afrika wafungwa mjini Addis Ababa
2022-02-04 17:26:29| CRI

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika (AU) wamemaliza kikao cha 40 cha kawaida cha Baraza tendaji la Umoja wa Afrika, kilichofanyika mjini Addis Ababa.

Athari mbaya za janga la COVID-19, kuongezeka kwa tishio la ukosefu wa usalama kutokana na migogoro na ugaidi, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika bara la Afrika ndio ajenda zilizotawala katika mkutano huo wa siku mbili.

Kwenye mkutano huo wa kwanza wa ana kwa ana tangu kutokea kwa janga la COVID-19, mawaziri wamesisitiza kuwa maendeleo katika chanjo dhidi ya COVID-19 ni ya polepole, na kutaka chanjo kuwafikia waafrika wote kuwa kipaumbele kwa Umoja wa Afrika.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya AU Bw. Moussa Faki Mahamat alibainisha kuwa bara la Afrika linahitaji dola za kimarekani bilioni 454 ili kukabiliana na msukosuko wa kiuchumi unaosababishwa na janga hilo.