Kenya na FAO waanzisha mkakati wa usimamizi wa wadudu wavamizi na magugu
2022-02-08 09:44:23| CRI

Kenya ikishirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO jana Jumatatu walizindua mkakati wa usimamazi wa wadudu wavamizi na magugu ili kuongeza usalama wa chakula na lishe nchini humo.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Ushirikiano, Peter Munya amesema mkakati wa wadudu wahamiaji na wavamizi nchini Kenya wa mwaka 2022-2027 utaboresha uwezo wa binadamu, ufuatiliaji na mfumo wa tahadhari ya mapema. Amesema wadudu hao wameleta changamoto kubwa katika Afrika Mashariki na kuleta athari mbaya kwa mazingira, usalama wa chakula wa taifa na maisha ya wakulima.

Akitolea mfano wa uvamizi wa nzige wa jangwani ulioshuhudiwa nchini Kenya kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita, Waziri Munya amesema umesababisha tishio kubwa la ukosefu wa chakula kwa watu zaidi ya milioni 4 wa kaunti 32 za Kenya.