Askari wa kulinda amani wa UM na jeshi la DRC waongeza doria karibu na eneo la shambulizi baya nchini DRC
2022-02-09 09:46:51| CRI

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema, walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo DRC waliongeza doria karibu na eneo la shambulizi baya lililotokea wiki iliyopita dhidi ya wakimbizi wa ndani IDPs lililoko mkoani Ituri, kaskazini mashariki mwa DRC.

Dujarric amesema walinzi wa amani wa huko wameeleza kuwa bado kuna hali ya wasiwasi katika Jimbo la Ituri baada ya shambulizi hilo, na imeripotiwa kuwa kuna watu waliokimbia makazi yao wanaonekana kati ya Savo na Blue.

Guterres alilaani vikali shambulizi lililotokea Februari 1, ambalo limesababisha vifo vya raia zaidi ya 58, na wengine 36 kujeruhiwa.

Dujarric amesema wataendelea kushirikiana na gavana wa Ituri kutafuta mbinu za kukabiliana na hali hiyo, na kwamba walinzi wa haki za binadamu pia wanatoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuimarisha ulinzi wa amani wa raia, na kuhakikisha usalama wa watu waliokimbia makazi yao.