Kenya yazindua kituo cha saratani cha kaunti
2022-02-09 09:45:28| CRI

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta jana Jumanne alizindua kituo cha saratani cha kaunti katika Hospitali ya Rufaa ya Coast General iliyopo Mombasa Kenya.

Kenyatta amesema kituo hicho ambacho kitahudumia wagonjwa wa saratani katika kaunti hiyo na nje ya kaunti, ni kituo cha pili cha aina hiyo nchini Kenya baada ya kile cha Hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Utafiti cha Kenyatta. Kituo hicho cha kisasa kabisa, ambacho kimeendelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali kuu na ya kaunti ya Mombasa kama nguzo ya mwongozo wa maendeleo ya Mpango wa Afya kwa Wote (UHC), kimewekewa vifaa vya teknolojia ya juu ili kutoa huduma za kina za saratani. Kenyatta amepongeza ushirikiano kati ya serikali kuu na za kaunti katika kutoa huduma za afya kwa Wakenya.

Naye Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema kuanzishwa kwa kituo maalumu cha saratani ni sehemu ya malengo ya rais ya Mpango wa UHC wa kuhakikisha Wakenya wanapata huduma nzuri za afya kwa gharama nafuu. Pia amesema mwezi ujao kituo kama hicho kitazinduliwa huko Nakuru vikifuatia na vituo vya kaunti za Garissa, Kisumu na Nyeri.