Shirika la misaada la Umoja wa Mataifa, limesema washirika wa Umoja wa Mataifa wameomba zaidi ya shilingi bilioni 500, sawa na dola bilioni 4.4 za Marekani ili kusaidia kuokoa maisha na kulinda watu milioni 29.1 nchini Ethiopia, Kenya na Somalia katika mwaka 2022.
Ofisi ya Uratibu wa Mambo ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (UNOCHA) imesema kati ya watu milioni 12 na 14 wanaamka kila siku wakikabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula na maji katika nchi zote tatu, kutokana na ukame katika robo ya kwanza ya mwaka huu. Shirika hilo limewataka wafadhili kuchangia mtandao wa wenyeji, jamii na mashirika ya wanawake, yakiwemo mashirika yanayoongozwa na wakimbizi, ambayo yanafanya kazi nzuri katika jamii zilizoathirika na ukame kila siku.
Kwa mujibu wa UNOCHA, kiasi cha watoto milioni 5.5 wanatarajiwa kuwa na utapiamlo mkali katika nchi hizi tatu ndani ya mwaka 2022, pamoja na zaidi ya milioni 1.6 ambao watakuwa utapiamlo mkali zaidi.