Kenya kuhimiza usalama wa chakula kwa kuongeza mauzo ya nje ya bidhaa za kilimo
2022-02-17 09:14:29| cri

Kenya inapanga kuinua kiwango cha usalama wa chakula kwa kuongeza mauzo ya nje ya bidhaa za kilimo. Ofisa mwandamizi wa wizara ya kilimo ya nchi hiyo Bw. Joseph Kirubi, amesema juhudi za serikali katika kuhimiza usalama wa chakula zitaendana na makubaliano ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Biashara Duniani(WTO).

Takwimu zinaonesha kuwa mauzo ya nje ya chakula yanachukua zaidi ya asilimia 50 ya jumla ya mauzo nje ya Kenya. Bw. Kirubi amesema kuboresha mfumo wa usalama wa chakula kutasaidia kuhakikisha bidhaa zake za kilimo hazizuiwi mipakani kutokana na kutokidhi viwango vya usalama wa Chakula.

Ameeleza kuwa hali ya kuongezeka kwa mahitaji ya chakula na kupungua kwa ardhi na maji kumehimiza matumizi ya bidhaa za teknolojia za kilimo na kuimarisha biashara inayohitaji usimamizi unaofaa wa hatari za kibaiolojia na kikemikali kwa usalama wa chakula.