Takwimu za nusu mwaka za Uganda zaonesha uchumi kuanza kufufuka kutokana na athari za COVID-19
2022-03-03 10:01:23| CRI

Uchumi wa Uganda umeonesha dalili za kufufuka katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 licha ya athari za virusi vipya vya COVID-19 katika kipindi hicho.

Kwa mujibu wa ripoti ya uchumi ya nusu mwaka iliyotolewa na Wizara ya fedha, ambayo inaanzia Julai 2021 hadi Disemba 2021, viashiria vya mara kwa mara vya shughuli za uchumi vinaonesha kuendelea kufufuka kwa shughuli za biashara. Viashiria hivyo ni pamoja na Kielezo Mchanganyiko cha Shughuli za Uchumi (CIEA), Kielezo cha Usimamizi wa Manunuzi (PMI) na Kielelezo cha Mwelekeo wa Biashara (BTI) ambavyo vinaonesha kwamba ingawa kulikuwa na hali ngumu ya uchumi katika mwezi Julai wakati uchumi ulipoanza kufufuka kutokana na zuio la pili, lakini uchumi ulirejea tena kufufuka katika miezi iliyofuata.

Ripoti inaonesha kuwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha ilishuhudia ukuaji wa asilimia 3.8, unaoonesha kuboreka kwa pato la taifa (GDP) ikilinganishwa na robo kama hiyo mwaka wa nyuma yake. Haya yamechangia kuongezeka kwa kasi ya ukuaji katika sekta zote mbili za viwanda na huduma.