Rwanda yahimiza matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme
2022-03-07 09:23:42| cri

Rwanda inaendelea na juhudi za kuhimiza matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati safi, na sasa katika mji mkuu Kigali ni kawaida kuona pikipiki zinazotumia betri.

Mwanzilishi na ofisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Ampersand inayotoa huduma ya pikipiki zinazotumia betri za kusafirisha abiria Bw. Josh Whale, amesema biashara yake inaendelea kwa kasi. Amesema kuwa mwanzoni alianza biashara hiyo kama majaribio mwaka 2016. Sasa anapanga kuongeza pikipiki zingine 450 kwenye biashara hiyo ili kufikia 500, zikiwemo 60 zitakazopelekwa Kenya mwezi ujao. Anatarajia kushuhudia pikipiki zote katika Afrika Mashariki ziwe zinatumia betri ifikapo mwaka 2030.

Mfumo wa betri unaotumika na kampuni hiyo utawarahisishia madereva kubadilisha betri za pikipiki zao katika vituo vyake vya kuchaji vinavyotumia umeme wa maji kutoka gridi ya taifa. Alisema bei ya pikipiki au magari yanayotumia betri ni ya chini na matumizi yake yanaweza kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa kwa asilimia 83.