Sudan Kusini yaadhimisha miaka miwili ya serikali ya umoja
2022-03-08 08:50:03| CRI

Sudan Kusini imeadhimisha miaka miwili ya serikali ya umoja, licha ya kukumbwa na mkwamo kwenye mambo ya katiba na kuendelea kwa vurugu za kikabila zinazochochewa na makundi yenye silaha na makundi ya kisiasa.

Naibu mwakilishi wa Umoja wa mataifa na mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS Bw. Nicholas Burns, amesema wakati imebaki miezi 12 ya kipindi cha mpito, wanakumbuka kuwa kuna mambo bado hayajatekelezwa na ni muhimu yakitekelezwa katika muda mfupi uliopo.

Ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kukamilika kwa teuzi tendaji katika ngazi za taifa na majimbo, na kuundwa upya kwa bunge la taifa na mpito, na mabaraza ya majimbo.

Ametaja mambo ambayo bado hayajatekelezwa kuwa ni pamoja na yale yanayohusu uhuru wa kisiasa na kiraia, mazingira salama, na matakwa ya kiufundi na kiugavi ya kufanya uchaguzi huru na wa haki.