Tanzania yarekodi ukuaji imara katika sekta ya madini mwaka 2021
2022-03-11 10:09:43| CRI

Waziri wa madini wa Tanzania Bw. Doto Biteko amesema, mchango wa sekta ya madini ya Tanzania katika uchumi wa taifa umeongezeka hadi asilimia 7.3 ya mwaka 2021 kutoka asilimia 6.5 ya mwaka 2020.

Bw. Biteko amesema makadirio ya serikali ni kushuhudia sekta ya madini kuchangia asilimia 10 ya uchumi wa nchi hiyo hadi mwaka 2025, na lengo hilo litatimizwa mapema zaidi.

Amesema hayo katika mkutano na wanahabari uliofanyika huko Dodoma, huku akisema sekta ya madini imeweka historia katika mwaka uliopita, wakati mauzo ya madini yakifikia shilingi trilioni 8.3 za Tanzania na serikali ikikusanya shilingi bilioni 597.53 za Tanzania katika kodi na utoaji wa idhini.

Pia ameongeza kuwa ushiriki wa watanzania katika huduma za sekta ya madini umeongezeka kutoka asilimia 43 hadi 63, wakati pato la huduma za madini likifikia dola milioni 579.3 za kimarekani.