Ofisa wa AU asema Afrika yatakiwa kutumia fursa ya maendeleo ya kasi ya soko la kidijitali
2022-03-16 08:46:18| CRI

Naibu mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika (AU) Monique Nsanzabaganwa amesema, Afrika inatakiwa kutumia fursa ya maendeleo ya kasi ya soko la kidijitali ili kuboresha upatikanaji wa bidhaa na huduma ndani ya bara hilo.

Bi. Nsanzabaganwa amesema hayo jana jumanne katika maadhimisho ya 39 ya Siku ya Kimataifa ya Kulinda Haki na Maslahi ya Wateja inayoadhimishwa kila Machi 15, chini ya kaulimbiu ya “Usawa wa Fedha za Kidijitali.”

Kutokana na matumizi ya mtandao barani Afrika kufikia asilimia 43, Bi. Nsanzabaganwa amesema uvumbuzi unabadili jinsi watu wanavyofanya malipo na kuishi maisha yao katika bara hilo, na kusisitiza kuwa fedha za kidijitali na maana yake katika ujumuishi wa kifedha na utulivu wa kifedha ni muhimu kwa maendeleo barani Afrika. Ameongeza kuwa, Afrika imeshuhudia ongezeko kubwa la huduma za kifedha za kidijitali, lakini ameonya kuwa, watumiaji wa fedha za kidijitali wanakabiliwa sana na matukio ya kihalifu ikiwemo kuibiwa, kudanganywa, na matumizi mabaya ya data, mambo yaliyochochewa zaidi na mlipuko wa janga la COVID-19.