Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa laongeza muda wa majukumu ya Kikosi chake nchini Sudan Kusini
2022-03-16 08:45:45| CRI

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuongeza muda wa majukumu ya Kikosi cha Ulinzi wa Amani cha Umoja huo nchini Sudan Kusini (UNMISS) kwa mwaka mmoja zaidi, mpaka tarehe 15 Machi, 2023.

Azimio hilo namba 2625 limeeleza utayari wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanya marekebisho ya ngazi za vikosi vya UNMISS na kazi za kujenga uwezo ili kuendana na mahitaji ya usalama nchini humo.

Pia, pamoja na mambo mengine, azimio hilo limeamua kuwa, majukumu ya UNMISS yanapangwa kuendeleza lengo la mkakati wa miaka mitatu ili kuzuia kurudi kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini, kujenga amani ya kudumu katika ngazi ya mkoa na taifa, na kuunga mkono ujumuishi na uwajibikaji wa serikali, na pia uchaguzi wa haki, huru na amani, kuendana na Makubaliano ya Ufufukaji ya mwaka 2018 kuhusu Utatuzi wa Mgogoro nchini Sudan Kusini.